Watanzania

Utangulizi

Ukurasa huu umeanzishwa maalum kwa Watanzania waishio Marekani, na Wamarekani wenye asili ya Tanzania.

Nchi ya Marekani ni kubwa, na ni vigumu Maafisa wa Ubalozi kumfikia kila Mtanzania huko aliko. Kwa bahati, TEKNOHAMA sasa inatuwezesha kuwasiliana hata bila kutembeleana. Tutatumia ukurasa huu pia kutoa matangazo na taarifa mbali mbali kwa Watanzania waishio Marekani.

Ubalozi huu upo kwa ajili yenu na tungependa tuunganishe Jumuiya ya Watanzania waliopo Marekani kimtandao na tutoe fursa ya kuchangia mambo ya kimsingi na kimaendeleo kwetu na kwa nchi yetu.

Kwenye ukurasa huu kuna eneo la jumla la kujiandikisha, ili ubalozi ujue mlipo na namna ya kuwafikia na kuwasiliana nanyi. Lipo pia eneo la wasomi na wanataaluma kujiorodhesha wakipenda na kueleza wasifu wao, na maeneo waliyobobea kitaaluma.

Ubalozi huu unaamini kuwa wapo Watanzania wengi waliosoma vizuri na kubobea kwenye fani mbalimbali za kitaaluma. Huu ni utajiri wa nguvu-kazi ya taifa letu, na hazina inayoweza kutumiwa na Serikali yetu, au makampuni binafsi yanayowekeza nchini mwetu.

Kujiandikisha kwenye orodha ya wanataaluma ni jambo la hiari kabisa. Kila anayejiandikisha atapewa uhuru wa kutoa kibali au kukataa wasifu wake kupelekwa Serikalini au kwa makampuni binafsi.

Tutatoa pia fursa kwa kila mtu kutoa maoni yake jinsi gani Watanzania walio Marekani wanaweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu kwa kutumia uzoefu wao wa kuishi kwenye nchi hii yenye uchumi mnkubwa kuliko zote.

Kwa pamoja, kwa kushirikiana, tutajenga nchi yetu.

Ombeni Sefue
BALOZI

Wanainchi